Waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wametangaza usitishaji wa mapigano kuanzia leo Jumanne huko mashariki mwa Kongo kwa sababu za kibinadamu.
Haya yanafuatia miito ya njia salama ya misaada kutolewa kwa maelfu ya watu walioachwa bila makao.
Tangazo hilo la waasi hao limekuja muda mfupi baada ya Shirika la Afya Duniani WHO kusema kuwa karibu watu 900 wameuawa kutokana na mapigano ya wiki iliyopita kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo.
Shirika la Uratibu wa Misaada ya Kiutu la Umoja wa Mataifa – OCHA limesema, idadi hiyo ya watu 900 iliyotangazwa na WHO katika ripoti yake, haijumuishi miili ya watu waliouawa kutokana na vita hivyo, iliyo katika vyumba vya kuhifadhia maiti.
Inaripotiwa kwamba miili ya watu bado imetapakaa katika mitaa ya mji wa Goma. Ripoti ya WHO pia inasema kulingana na mamlaka za mji huo, watu 2,900 walijeruhiwa kutokana na mapigano hayo.
Tangazo hilo la usitishwaji mapigano pia linakuja kuelekea mkutano wa kilele wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya SADC wiki hii ambapo Rais William Ruto wa Kenya amethibitisha kwamba Rais Paul Kagame wa Rwanda na mwenzake wa Kongo Felix Tshisekedi watahudhuria mkutano huo.
Viongozi wote wawili wamekuwa wakikwepa kuhudhuria mikutano ya awali ya kutafuta amani katika mzozo unaoendelea nchini Kongo.
Mamlaka nchini Kongo zimesema ziko tayari kwa mazungumzo ya kuleta amani ila mazungumzo hayo ni sharti yafanyike kwa muktadha wa makubaliano yaliyopita.
Mji wa Goma wenye idadi ya watu milioni 2 uko katikati ya eneo lenye utajiri wa madini na unasalia kuwa chini ya udhibiti wa waasi. M23 wameripotiwa kusonga mbele na kuchukua udhibiti wa maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo.