You are currently viewing Rais Kagame aionya Afrika Kusini

Rais Kagame aionya Afrika Kusini

Serikali za Afrika Kusini na Rwanda zimeingia katika mzozo kutokana na vita vinavyoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya wanajeshi 13 wa Afrika Kusini kuuawa katika uwanja wa mapambano.

Kufuatia vifo hivyo, serikali ya Afrika Kusini imetoa taarifa kupitia mtandao wake wa kijamii wa X (Twitter), ikitoa salamu za pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuishutumu Rwanda kwa kushirikiana na waasi wa M23 katika mashambulizi hayo.

Baada ya tamko hilo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame jana Jumatano alikanusha tuhuma hizo, akizitaja kuwa za uongo na kinyume na mazungumzo aliyokuwa nayo na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. 

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Kagame alidai kuwa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) si kikundi cha waasi bali ni jeshi rasmi la Rwanda, akidai kuwa misheni ya SADC nchini DRC (SAMIDRC) inalenga kushambulia wananchi wa DRC na kuivamia Rwanda kijeshi.

“Wapendwa Wananchi wa Afrika Kusini, kutokana na kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa DRC, tumepoteza wanajeshi wetu 13 shujaa waliokuwa wakipigania amani.

Mapigano haya yamechochewa na waasi wa M23 kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) dhidi ya Vikosi vya FARDC na walinda amani wa Misheni ya SADC (SAMIDRC).

“Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Afrika Kusini, tunatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na tunawaenzi kwa ujasiri wao. Msaada wote muhimu unapatikana kwa familia zilizoathirika, huku taratibu za kuwarejesha nyumbani waliofariki zikiendelea.

Mashambulizi haya yameathiri pia wanajeshi kutoka Malawi, Tanzania, na wanachama wa MONUSCO. Hali katika Goma na Sake bado hali ni tete na isiyotabirika, lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha vikosi vya SAMIDRC vinapokea msaada wa kutosha.

“Uwepo wa wanajeshi wetu mashariki mwa DRC haupaswi kutafsiriwa kama tangazo la vita dhidi ya taifa lolote, bali ni juhudi za kuleta amani chini ya Umoja wa Mataifa na SADC. Tunasisitiza pande zote kushiriki juhudi za kidiplomasia ili kupata suluhisho la kudumu,” ilisema taarifa iliyotolewa ba Serikali ya Afrika Kusini.

Rais Kagame alijibu madai ya Afrika Kusini kwa kusema: “Nimefanya mazungumzo na Rais Ramaphosa kuhusu hali mashariki mwa DRC, lakini taarifa zinazotolewa na maafisa wa Afrika Kusini ni potofu na za upotoshaji.

“Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) ni jeshi rasmi, si kikundi cha waasi. SAMIDRC si kikosi cha ulinzi wa amani bali ni jeshi la mashambulizi lililotumwa kusaidia serikali ya DRC kupigana dhidi ya raia wake, likishirikiana na vikundi vya kigaidi kama FDLR ambavyo vinatishia usalama wa Rwanda.

“SAMIDRC ilihusika na kuondolewa kwa Vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, jambo ambalo limehujumu juhudi za mazungumzo ya amani. Rais Ramaphosa hakutoa onyo lolote dhidi ya Rwanda, bali aliomba msaada wa chakula, maji, na umeme kwa wanajeshi wake.

“Wanajeshi wa Afrika Kusini hawakuuawa na M23, bali waliuawa na vikosi vya FARDC. Ikiwa Afrika Kusini inataka kusaidia amani, tunakaribisha juhudi hizo. Lakini kama wanataka mzozo, Rwanda iko tayari kukabiliana nao,” amesema Kagame.

Leave a Reply