RAIS Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Sorngwe, Bi. Esther Alexander Mahawe kilichotokea leo tarehe 14 Januari, 2025 katika hospitali ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Rais Samia ametoa pole familia ya marehemu, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Bi. Esther na utumishi wake kwa umma ambao uliongozwa na uchapakazi hodari, ukweli na msimamo thabiti katika utendaji.
“Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina,” ameandika Rais Samia.
Esther aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kigoma Juni 2021 kisha Januari 2023 alimhamishia wilayani Mbozi mkoani Songwe alikotumikia hadi umauti ulipomfika.