You are currently viewing LALJI FOUNDATION yagawa vifaa vya shule kwa vituo tisa vya watoto yatima Dar

LALJI FOUNDATION yagawa vifaa vya shule kwa vituo tisa vya watoto yatima Dar

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wazazi na walezi nchini wamekumbushwa kuzingatia jukumu la kulea watoto katika ngazi ya familia ili wapate huduma za malezi bora  na upendo wa dhati kutoka kwa baba na mama pamoja na ndugu wa karibu.

Wito huo umetolewa jana Alhamisi na Naibu Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamis wakati wa hafla ya kukabidhi sare na vifaa vya shule kwa  vituo tisa vya makao ya kulea  watoto yatima jijini Dar es salaam vilivyotolewa na Taasisi ya LALJI FOUNDATION. 

“Sio kila mtoto anayelelewa katika vituo vya kulea watoto yatima hana wazazi bali kuna sababu mbalimbali ambazo zinapelekea watoto kulelewa katika vituo hivyo, lakini watoto wakilelewa katika ngazi ya familia itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaolelewa katika vituo hivi”  amesema.

Aidha, ameipongeza taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kuboresha mazingira ya sekta ya elimu nchini huku akitoa wito kwa wadau wengine kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye uhitaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya LALJI FOUNDATION, Imtiaz Lalji amesema lengo la taasisi hiyo ni kuendelea kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji na  akibainisha kuwa msaada huo waliotoa kwa Watoto yatima utawawezesha kielimu .

“Tunaelewa kuwa upatikanaji wa elimu na rasilimali muhimu kama vifaa vya shule ni nyenzo muhimu sana katika kufungua fursa za watoto kutimiza ndoto zao hivyo basi hiyo ndo sababu kubwa ambayo imetupelekea kusaidia Watoto hawa kupata vifaa wanavyohitaji kufikia malengo yao ya elimu” amesema. 

Aidha, ameishukuru serikali kwa kuweka mazingira bora kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo taasisi ya LALJI FOUNDATION kufanya kazi za kijamii kwa utulivu na ushirikiano mkubwa kutoka serikalini.

Vilevile Imtiaz amepongeza juhudi na kazi kubwa inayofanywa na wasimamizi wa vituo vya kulea Watoto yatima nchini kwa kujitolea muda na nguvu zao katika kulea Watoto hao.

Akizungumza kwa niaba ya walezi wa vituo tisa vya kulelea Watoto yatima ambavyo vimepatiwa msaada huo Mama Mutemwa kutoka kituo cha kulea Watoto cha Bibi na Babu ameishukuru taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kutoa msaada huo kwani utasaidia Watoto hao kuhudhuria masomo bila changamoto ya vifaa na itawasaidia kutimiza doto zao huku akitoa wito kwa wadau wengine kuendelea kupeleka misaada kwani uhitaji bado ni mkubwa.

Naye Katibu wa LALJI FOUNDATION, Fatema Lalji amesema jumla ya Watoto 400 kutoka makao 9 ya kulea Watoto yatima Dar es salaam wamepatiwa msaada huo na kubainisha kuwa taasisi hiyo inasaidia vituo vya Watoto yatima kila mwisho wa mwaka kwa kuwapa sare za shule , mabegi, viatu, soksi kupitia mradi huo endelevu ambao unatekelezwa kila mwaka .

Leave a Reply