Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palanagamba Kabudi ameeleza kusikitishwa na vitendo vya mashabiki kung’oa na kuharibu viti vya kukalia watazamaji katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jjini Dar es Salaam katika mchezo wa kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba Sport Club ya Tanzania na Club Sportif Sfaxien ya Tunisia uliofanyika jana tarehe 15 Desemba, 2024.
Prof. Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuchukua hatua mara moja kwa kuwaandikia timu ya Simba Sports Club na kuwanakili Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) ili gharama za uharibifu uliosababishwa wakati mechi hiyo zilipwe.
Waziri Kabudi amewataka mashabiki wanaoingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.
“Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubaliki na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja nakuwaandikla Simba Sports Club na TFF, wapeni ushirlkiano Polisi ili watu wote waliokuwa wanang’oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisherla, lazima tabia hii ikomeshwe” amesema Prof. Kabudi.