You are currently viewing Rais Biden, Trump kujadili vita vya Ukraine

Rais Biden, Trump kujadili vita vya Ukraine

Rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa kujadiliana na Rais mteule Donald Trump kuhusu vipaumbele vya sera za ndani na nje, wakati watakapokutana keshokutwa Jumatano huku suala la vita vya Ukraine ikiwa ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa.

Mshauri wa masuala ya Usalama wa Taifa, Jake Sullivan amesema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa Biden anatarajiwa kutoa wito Trump kutoiacha Ukraine.

Kwenye mahojiano na kituo cha utangazaji cha CBS, Sullivan amesema ujumbe muhimu wa Biden utajikita katika makabidhiano ya amani ya madaraka, lakini pia atamweleza Trump kile kinachoendelea barani Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati.

“Rais atakuwa na nafasi ya kumuelezea Rais mteule Trump juu ya namna anavyoyaangazia mambo, msimamo wake na namna Trump atakavyoshughulikia masuala hayo atakapoingia madarakani.” alisema Sullivan.

Ingawa Sullivan hakufafanua kwa kina ni maeneo gani hasa yatagusiwa, lakini huenda wakajikita kwenye vita vya Urusi na Ukraine, ambavyo Trump ameahidi kuvimaliza mara moja, ingawa bado hajasema ni kwa namna gani.

Washington tayari imetoa msaada wa mabilioni ya dola kuisaidia Ukraine kijeshi na kiuchumi, tangu ilipovamiwa na Urusi, Februari 2022, lakini mara kwa mara Trump amekuwa akikosoa hatua hiyo.

Sullivan anatoa matamshi hayo wakati Ukraine ikiishambulia Moscow siku ya Jumapili kwa droni karibu 34, hilo likiwa ni shambulizi kubwa kabisa la droni kwenye mji mkuu wa Urusi tangu kuanza kwa vita hivyo.

Huku hayo yakiendelea, Rais mteule wa Marekani Donald Trump anaarifiwa kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kumtolea wito wa kutovízidisha vita nchini Ukraine, gazeti la Washington Post limearifu jana Jumapili.

Trump alizungumza kwa simu na Putin kutokea kwenye makazi yake ya Mar-a-Lago, Florida siku ya Alhamisi, siku moja baada ya kushinda uchaguzi.

Leave a Reply