You are currently viewing Sagini ipongeza RITA kuwanoa ma-DAS, maofisa ustawi wa jamii
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini

Sagini ipongeza RITA kuwanoa ma-DAS, maofisa ustawi wa jamii

Katika jitihada za kupunguza migogoro isiyo na ulazima katika jamii, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ameupongeza Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kutoa mafunzo ya umuhimu wa kuandika wosia na kufanya usajili wa vizazi na vifo kwa Makatibu Tawala wa Wilaya na Maofisa Ustawi wa Jamii  katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili waweze kuielemisha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya hivyo.

“Changamoto za masuala ya mirathi bado zipo katika jamii yetu ambapo wajane na warithi halali hupoteza haki zao mara baada ya mzazi mmoja na hasa baba anapofariki,hivyo ni vema kutoa elimu na kuwashauri wananchi kuandika Wosia hata wakati wakiwa bado hai,” amesema Naibu WAZIRI Sagini wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo katika  kijiji cha Kyabakari wilayani Butiama mkoani Mara.

Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bw Frank Kanyusi akizungumza na Makatibu Tawala wa Wilaya na Maofisa Ustawi wa Jamii katika halmashauri zote za mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Geita,Simiyu na Shinyanga,  ( hawapo pichani ) wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo kuhusu huduma zinazotolewa RITA, iliyofanyika jana wilayani Butiama Mkoani Mara.

Amesema kuwa wosia husaidia kuondoa migororo, wakati usajili wa matukio ya vizazi na vifo, ndoa (zikiwemo za kimila) na talaka ni muhimu kwa wananchi kwani huwawezesha kupata huduma nyingine muhimu za kijamii ikiwemo huduma za afya, ajira, kitambulisho cha Taifa na kitambulisho cha kupigia kura.

Hivyo, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa (mikoa ya Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga na Simiyu) kulifanya jambo hili ajenda katika mikutano yao na  kutoa elimu kwa jamii ili mpango huu uweze kufanikiwa.

“Takwimu zinazopatikana baada ya usajili zinaisaidia Serikali katika kupanga mipango ya maendeleo na huduma za kijamii;”

“Hivyo, naipongeza RITA kuandaa mafunzo haya muhimu ambayo kama Serikali tunaona yataleta mabadiliko makubwa kwa kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi,” amesema.

Pia ameipongeza RITA kwa kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ambayo imesaidia kuongeza kasi ya usajili ikiwemo kubuni mfumo wa kidijitali (eRITA) ambao unawawezesha wananchi kutuma maombi na kupata huduma kidijitali bila hata kufika katika ofisi za RITA.

“Matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma ni  azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka wananchi wapate huduma bila usumbufu wowote,” amesema.

Akiongea kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw Frank Kanyusi   amesema RITA  imekuwa ikiandaa mafunzo na vikao na wadau wa makundi mbalimbali,  kwa ajili ya kuwajengea uwezo, kubadilishana uzoefu, kuibua na kujadili changamoto na kujadiliana namna bora ya  kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Pia amesema kuwa mafunzo hayo kwa kiasi kikubwa yamegusia juu ya umuhimu wa ndoa za kimila, ambapo RITA itaweka mkakati madhubuti wa kuziweyesha ndoa hizo kusajiliwa ili kupata takwimu zake sahihi.

Pia amegusia maendeleo ya mpango wa kuwasajili watoto walio chini ya miaka mitano unaotekelezwa katika mikoa yote 26 Tanzania Bara ambao umewezesha takriban watoto milioni 10.3 kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, umeongeza vituo vya usajili kutoka 135 mwaka 2013 hadi kufikia vituo 11,257 mwaka 2023 katika halmashauri 184 zinazohusisha watendaji kata 3,957 na vituo 7,116 vinavyotoa huduma za baba, mama na mtoto.

“Haya ni mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kutokana na uratibu wa Maofisa Ustawi wa Jamii ambao wamepewa mafunzo na RITA,” amesema Kanyusi.

Leave a Reply