Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango Makamu wa Rais ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) pamoja na Watalaam wa fikra tunduizi kufanya utafiti kuhusu tabia za hivi karibuni za vijana kushiriki katika mahusiano na wanawake waliowazidi umri maarufu (mashangazi) kama njia rahisi ya kujikimu, kutumia muda mwingi bila kufanya kazi kwa kushinda vijiweni, uchezaji kamari, utupaji taka ovyo, uchomaji moto ovyo wa nyasi na misitu pamoja na ubinafsi.
Pia amesema zinahitajika tafiti za kina pamoja mikakati katika kufanya mapinduzi ya kitamaduni kubadili tabia na mazoea yasioyafaa yanayojitokeza katika jamii hivi sasa ambayo ni kikwazo kwa maendeleo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kusherehekea Miaka 30 ya Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) uliofanyika jana Jumatatu Jijini Dar es Salaam.
Ametaja baadhi ya mazoea na tabia hizo ni pamoja na kutojali muda, kutokuwa na uaminifu mahali pa kazi pamoja na kutumia njia zisizofaa katika kupata kipato.
Pia Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuangazia tabia zingine kama vile matumizi makubwa ya fedha katika anasa kuliko kuweka akiba ikiwemo uchangiaji zaidi katika matukio ya sherehe na tafrija kuliko kusaidia gharama za elimu na matibabu kwa familia za kipato cha chini.
Mengine ni kuongezeka kwa tabia ya utegemezi pamoja na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake, watoto pamoja na vitendo vya ushirikina ikiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa ESRF kufanya tafiti katika maeneo mengine muhimu ikiwemo hatari za kimataifa kama vile mabadiliko ya haraka ya Teknolojia, kutokuwa na uchumi stamihilivu, mizozo mikali inayopelekea mivutano ya kisiasa pamoja na kufanya tafiti kufahamu mienendo ya soko la ajira na namna vijana watakavyoweza kuendana nayo.
Amesema ili kutumia vema idadi kubwa ya vijana iliyopo barani Afrika ikiwemo Tanzania, Taasisi za Tafiti zinapaswa kuanisha ufadhili endelevu wa miradi na programu zinazopendelewa na vijana kulingana na vipaumbele vya Taifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa tafiti katika sekta ya madini ikiwemo madini adimu ya kimkakati ambayo ni msingi wa viwanda vya teknolojia ya juu, tafiti juu ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwa njia endelevu pamoja na tafiti zitakazolenga kufanya mageuzi ya maeneo yanayotambulika kama nusu jangwa kuwa fursa mpya ya uzalishaji nchini.
Amesema zinahitajika tafiti za maendeleo ya kilimo kwa kutumia maji yaliyopo chini ya ardhi pamoja na uvunaji maji ili kuleta mabadiliko katika maeneo hayo.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendelea kufanya kazi na kusaidia utafiti wa kiuchumi na uchambuzi wa sera unaofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) pamoja na taasisi nyingine za ndani ikiwa lengo ni kuongeza ufadhili wa utafiti na uwekezaji katika miundombinu inayounga mkono tafiti hizo.
Amesema Serikali itaendelea kusisitiza Wizara, Idara na Wakala mbalimbali kutumia huduma zinazotolewa na ESRF ili kuhabarisha maendeleo ya sera na mikakati ya kisekta. Pia ameongeza kwamba Serikali itaendelea kuhimiza sekta binafsi, Azaki, Wadau wa Maendeleo na wadau wengine kuendelea kushirikiana na ESRF.
Mkutano huo, umehudhuriwa na watafiti, wasomi, watunga sera, wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) wa sasa na zamani.