You are currently viewing Rais Ruto amteua Kindiki kumrithi Gachagua

Rais Ruto amteua Kindiki kumrithi Gachagua

Rais wa Kenya, William Ruto amemteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mpya kufuatia kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua jana Alhamisi usiku.

Jina la Kindiki limewasilishwa bungeni leo Ijumaa asubuhi ambapo wabunge wanatarajiwa kulipigia kura kuidhinisha.

Prof. Kithure Kindiki

Spika Moses Wetang’ula alitangaza uteuzi huo katika kikao maalum kilichoandaliwa Ijumaa asubuhi.

“Nimepokea ujumbe kutoka kwa rais kuhusu uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kujaza nafasi katika afisi ya Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” Wetang’ula alitangaza.

Katiba inasema pindi rais akishawasilisha uteuzi kwenye Bunge, wabunge watapiga kura ya kulikataa au kuliidhinisha jina hilo. Pia hakuna sharti la kura ya theluthi mbili.

Kisha mteule ataapishwa kuwa ofisini baada ya kuidhinishwa.

Kindiki amekuwa akihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani kwa takriban miaka miwili.

Hapo awali alihudumu kama Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi kwa mihula miwili ya miaka 10.

Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022, Kindiki alikuwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto lakini hatimaye akaamua kumchagua Gachagua.

Baadaye rais alieleza kwamba alimchagua Gachagua kwa sababu ya umri wake na alifikiri wangeelewana zaidi.

Prof. Kithure Kindiki ambaye ni msomi wa Sheria kutoka Kijiji Maskini sana, ni mtoto wa  tano kuzaliwa kati ya watoto nane wa familia ambayo baba yake ni mtumishi wa  Mungu.

Kindiki amewahi kuwa Gavana wa Tharaka – Nithi, Naibu Spika mstaafu wa Senate, Wakili wa Ruto katika kesi ya ICC.

Leave a Reply